Home Back

Shigongo: Nafanya masters kwa kutumia kipaji pekee

mwanahalisionline.com 2024/7/7
Eric Shigongo

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo (CCM) ameishukuru Serikali kwa kurejesha utaratibu wa kutambua maarifa yaliyopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (Recognition of Prior Learning) kwani yeye ni tunda la mmoja wa Watanzania walioendelea na masomo ya elimu ya juu kwa kutumia kipaji pekee. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

“Shukrani kubwa kwa serikali kwa sababu nilipoingia bungeni hapa kwa mara ya kwanza haya yalikuwa mapambano yangu ili watu wenye ujuzi nje ya shule wapatiwe nafasi ya kusoma na mimi ni tunda la watu ambao wamepata nafasi hiyo… sasa hivi nafanya masters ya mass communication kwa kutumia kipaji peke yake,” amesema.

Omar Kipanga

Shigongo ametoa shukrani hizo leo Ijumaa bungeni jijini Dodoma baada ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga kusema kwa sasa Serikali imeandaa Mwongozo wa Kutathmini na kutambua Maarifa yaliyopatikana nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning).

Akijibu swali la Shigongo kwamba lini Serikali itarejesha utaratibu huo, Kipanga amesema mwongozo huo unaweka utaratibu wa utambuzi na urasimishaji wa maarifa yaliyopatikana nje ya mfumo wa shule katika fani mbalimbali za amali kwa lengo la kuwawezesha walengwa kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa kazi.

“Kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, toleo 2023 ambapo mfumo wa kutambua na kurasimisha ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo umepewa kipaumbele, Serikali itatekeleza afua za kuimarisha utaratibu wa utambuzi na urasimishaji wa maarifa, ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo,” amesema.

Aidha, amesema elimu nje ya mfumo rasmi itatambuliwa, na watakaopitia mfumo huo watakuwa na fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu kulingana na vigezo vitakavyowekwa.

People are also reading