Home Back

Binti adaiwa kubakwa kisha kuuawa *Wanaodaiwa wapenzi wake wakamatwa

ippmedia.com 2024/10/5
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa.

MWILI wa binti mwenye umri wa miaka (17), mkazi wa Nyamanoro, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza umekutwa katika uchochoro ukiwa hauna nguo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, alisema jana kuwa mwili huo uligundulika Mei 27 mwaka huu saa 12 asubuhi katika Mtaa wa Nyamanoro Mashariki.

Alisema kuwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, askari wake walifika eneo la tukio na baada ya kukagua mwili huo, ilikutwa michubuko mgongoni na kwenye mkono wa kushoto.

Kamanda Mutafungwa alisema mwili huo ulipelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa (Sekou Toure) ambako uchunguzi wa awali ulibaini kuwa binti huyo aliuawa na mwili ulikutwa na dalili za kuingiliwa kimwili.

"Katika tukio hilo tunawashikilia watu wawili ambao ni Jovin Kamando (26), mkazi wa Kilimahewa jijini pamoja na Kelvini Raymond (27), mkazi wa Kitangiri jijini ambao wote wanasemekana walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti huyo," alisema Kamanda Mutafungwa.

Kwa umri wa miaka 17 aliokuwa nao binti huyo unamweka katika kundi la watoto. Sheria ya Ulinzi wa Mtoto ya Mwaka 2009 inazuia kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto.

Vilevile, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, inaelekeza adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani kwa anayekutwa na hatia ya kubaka mtoto au kifungo cha maisha gerezani kwa wanaobaki wakiwa katika kikundi.    

Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha tukio hilo kinasadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi na uchunguzi unaendelea. Ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Alisema Jeshi la Polisi linaomba wananchi wote wenye taarifa zozote juu ya tukio hilo waziwasilishe ndani ya jeshi hilo huku akitaka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na matukio ya mauaji.

Kamanda Mutafungwa pia alithibitisha jeshi hilo kushikilia watu sita kwa tuhuma za kumuua mama yao mzazi, Shija Magelanya (77) wakimtuhumu kuwaroga wajukuu zake na kuwasababishia wendawazimu.

Alisema tukio hilo lilitokea Juni Mosi mwaka huu saa 2:30 usiku katika Kijiji cha Nduwa, Kata ya Kasororo, wilayani Misungwi ambako bibi huyo, akiwa amekaa na wajukuu zake wakila chakula, ghafla walivamiwa na mwanaume aliyekuwa na panga kisha akaanza kumkata maeneo ya kichwani na mabegani na kusababisha kupoteza maisha papohapo.

"Chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina ambapo watoto wa bibi huyo wamekuwa wanamtuhumu mama yao kuroga wajukuu zake na kuwasababishia wendawazimu na hata vifo ambavyo vimekua havieleweki nyumbani kwao," alisema Kamanda Mutafungwa.

People are also reading