Home Back

Maabara kukuza TEHAMA PAPU

ippmedia.com 2024/10/5
NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi.

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi.

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, amezindua maabara ya kisasa kwa ajili ya kulisaidia Shirika la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kukuza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma.

Mahundi, alizindua  maabara hiyo ya kisasa yenye kompyuta 30 jijini Arusha juzi baada ya kufungua Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU linaloundwa na nchi 45 wanachama wa umoja huo. 

 Mkutano huo uliuhudhuriwa na wadau wa sekta ya Posta Barani Afrika na wajumbe wa Sekretarieti ya Umoja wa Posta Duniani. 

"Maabara hii itakuwa na tija kwa PAPU, likiwemo shirika letu la Posta nchini kutengeneza mifumo itakayoboresha mifumo ya Posta Afrika kuwa ya kidijitali na kufanya biashara za kimataifa ya kusafirisha vifurushi na vipeto kwa muda mfupi," alisema 

Kuhusu Baraza la Utawala la PAPU, alisema katika mkutano wao huo wa siku mbili watajadiliana namna bora ya kuboresha uendeshaji wa Posta Afrika.  

"Matumaini yangu kuwa kila nchi mwanachama wa PAPU tutaendelea kutumia mfumo wa kidijitali zaidi huduma zetu ambao utasaidia kufanya biashara mtandao katika ukanda wa nchi za Afrika na nje," alisema 

Awali Katibu Mkuu wa PAPU, Sifundo Moyo, alisema mkutano huo pia watapokea taarifa ya kamati nne za wataalamu ili kuweka mipango yenye manufaa kwa umoja huo. 

"Kamati hizo ni za fedha na utawala, uendeshaji na teknolojia, mikakati  na ya sera na kanuni. Tunaimani maoni na mapendekezo watakayoyawasilisha yatasaidia PAPU kusonga mbele zaidi hasa katika masuala ya teknolojia," alisema 

Posta Masta Mkuu, Maharage Chande, alisema uendeshaji wa huduma za posta kidijitali, utasaidia wananchi wa hali ya chini kufanya biashara kwa njia ya mtandao kwa kutumia shirika hilo kusafirisha vifurushi vyao ndani na nje ya nchi. 

"Shirika la Posta Afrika tumeanza kutengeneza duka mtandao ili kukuza huduma zetu kimataifa, lakini maabara iliyozinduliwa itawezesha wananchi wa hali ya chini kufanya biashara zao mtandao na watasafirisha biashara hizo kupitia shirika letu na Posta kupitia mfumo wetu wa kidijitali na biashara ya aina hii imeshika kasi kwa sasa," alisema Chande.

People are also reading