Home Back

Mama asimulia watu wasiojulikana walivyompora mwanawe mwenye ualbino

mwananchi.co.tz 2024/7/7

Muleba. Mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula wilayani Muleba mkoani Kagera, Judith Richard (20) amesimulia jinsi watu wasiojulikana walivyompora mtoto wake mwenye ualbino na kutokomea naye kusikojulikana.

Tukio la mtoto huyo wa kike, Asimwe Novath (2) kukwapuliwa mikononi mwa mama yake, lilitokea Alhamisi Mei 30, 2024, saa 1 jioni na msako wa kumtafuta mtoto huyo unaendelea.

Mwananchi Digital imefika hadi familia hiyo inapoishi na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wamekusanyika huku nyuso zao zikitawaliwa na huzuni.

Judith akiwa katika nyumba ya udongo anaonekana mwenye mawazo na macho yake yakibubujikwa machozi.

Tukio lilivyotokea

Judith amesema siku hiyo (Alhamisi) jioni baada ya kumaliza manunuzi dukani, alirejea nyumbani akiwa na mtoto wake, akiwa ndani ya nyumba alisikia sauti ya mwanaume aliyekuwa akiomba msaada wa chumvi.

Kwa mujibu wa Judith, mwanaume huyo aliyejitambulisha anaitwa Kennedy, alidai rafiki yake (jina halijatambulika) amegongwa na nyoka mguuni, hivyo anahitaji chumvi ili kupunguza maumivu kwenye jeraha hilo.

Amesema alipotoka nje aliwakutwa watu wawili, mmoja amesimama na mwingine amechuchumaa.

"Nilipoleta chumvi aliyekuwa amechuchumaa alinyanyuka na kunikaba, sikuweza kumuona vizuri maana simu niliyokuwa namulikia wakati nampatia chumvi alininyang'anya, halafu wa nyuma akamkwapua mtoto wangu wakatokomea naye kwenye migomba," anasema Judith.

Amesema baada ya kukwapuliwa mtoto wake, alipiga kelele (yowe) kuomba msaada kwa majirani ili kumsaidia kumtafuta mtoto wake, ndipo majirani walipokusanyika nyumbani kwake na kuanza msako huo ambao hata hivyo haukuzaa matunda.

Tukio hilo lilitokea akiwa peke yake, kwani mumewe Novath Asimwe (24), alibaki eneo walipofanya manunuzi na mkewe alipopaitacenter’,  hadi tukio lilipotokea.

Baada ya tukio hilo Judith alimwita jirani yake, Prisca Honorasco na kumweleza mkasa mzima ndipo aliposhauriwa kwenda kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji ambaye alianzisha msako huo.

"Baada ya Ofisa Mtendaji wa Kitongoji kuitisha msako, wakaanza kuzunguka maeneo yote wakitafuta lakini baada ya saa moja walirudi, wakawasha pikipiki na kwenda Kamachumu, wakaungana na wengine wakazidi kutafuta bila mafanikio."

"Ndipo Ofisa Mtendaji aliponishauri kwenda kutoa taarifa Polisi, tukaenda kutoa taarifa na (askari) wakaja eneo la tukio kuanza uchunguzi hadi leo mtoto hajapatikana. Naomba Serikali inisaidie kumpata mtoto wangu," amesema.

Tukio linaibua hofu

Jirani wa familia hiyo, Dickson Joas pamoja na kueleza kusikitishwa na tukio hilo, amesema linaibua hofu kwa watu wenye ualbino, hasa kipindi hiki nchi inapoelekea kipindi cha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

"Watu wenye ualbino wameumbwa kama sisi, ndiyo maana tunaomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina kujua sababu ya kuanza kurejea kwa matukio haya," amesema Joas.

Kauli ya Joas inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbale, Marchades Zephrine ambaye ameomba kuimarishwa ulinzi katika maeneo yenye kaya zenye watu wenye ualbino.

"Mazingira ya hii familia si rafiki kuishi na mtoto mwenye ualbino,  maana walikuwa ndio wamehamia muda si mrefu na majirani kaya zao ziko mbalimbali, huenda hiyo ikawa sababu ya watu hao kutekeleza tukio hilo bila kushtukiwa," amesema.

Baba mbaroni

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel amesema wanamshikilia baba wa mtoto huyo, Novath Asimwe (24) na wenzake wawili (majina yamehifadhiwa) wakidaiwa kuhusika.

"Mtoto bado hajapatikana ila tunaendelea na msako na mahojiano kwa watuhumiwa watatu akiwemo baba yake mzazi. Lengo ni kuhakikisha tunampata akiwa hai na kumrejesha katika familia yake na watuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria," amesema Daniel.

Kaimu Kamanda huyo ameenda mbali na kuitaka jamii kuachana na imani potofu huku akiiomba kutoa ushirikiano kwa Polisi ili kufanikisha kupatikana kwa mtoto huyo na kukamatwa kwa wahusika wote.

Ombi la TAS

Kufuatia tukio hilo, Makamu Mwenyekiti wa chama cha Watu wenye Ualbino nchini (TAS), Alfred Kapole amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi kuwasaka wahusika na kumrudisha mtoto huyo kwa wazazi wake akiwa hai kama inavyofanyika linapotokea tukio la wizi wa silaha au nyara za Serikali.

Kapole amesema mbali na kuwashtua, tukio hilo limeibua taharuki kwa watu wenye ualbino, jambo linaloweza kusababisha wasijiamini na kuachana na shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.

"Ni Jambo la kusikitisha kwamba Tanzania ni nchi yetu sote lakini mtoto huyu (Asimwe) tangu atekwe na watu hao hajapatikana wala watuhumiwa hawajakamatwa. Sasa tafsiri ya Tanzania ni nchi ya amani iko wapi?" alihoji.

"Tunaiita Tanzania kisiwa cha amani, haiwezi kuwa kisiwa cha amani kwa watu fulani wakati wengine hawana amani, ni sawa na kuwa na watoto saba,  unawanunulia nguo, mmoja unamuacha atajisikia vibaya. Tunakosa amani kwa jamii inayotuzunguka, ndoa zitavunjika, tumepanga katika majumba ya watu, tutafukuzwa na watu," amesema Kapole.

Amesema kuna matukio mengine ya watu wenye ualbino kushambuliwa, kunyofolewa viungo na kuuawa lakini Jeshi la Polisi halitoi taarifa ya hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa watuhumiwa.

"Kama Jeshi la Polisi wameshindwa kabisa kuwakamata na kutokomeza matukio ya aina hii basi waruhusu Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waingilie kati. Haiwezekani mtu anatoka huko anamnyang'anya mtu mtoto halafu tangu Alhamisi, hadi sasa hawajamkamata wala kumpata," amesema.

Kapole amesema matukio hayo yalianza kupotea, lakini yameanza kuibuka tena, hivyo ameiomba Serikali na mashirika yasiyo ya Serikali (NGO) kuongeza nguvu katika elimu dhidi ya imani potofu, kutokomezwa kwa wapiga ramli chonganishi na kuongezwa ulinzi kwa watu wenye ualbino nchini.

Kapole amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan akemee tukio hilo.

Matukio hayo ya ukatili, ukatwaji, au unyofolewaji viungo vya mwili, au ufukuliwaji makaburi na mauaji ya kinyama dhidi ya watu wenye ualbino yalianza kuripotiwa na vyombo vya habari katika kipindi cha miaka ya 2006 kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Juhudi mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Serikali, zikiwemo kuanzishwa kwa kambi za watu wenye ualbino ikiwemo kambi ya Kabannga (Kigoma), Buhangija (Shinyanga), Mitindo (Mwanza), Pongwe (Tanga), Kitengule (Tabora) na Mugeza (Kagera).

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye ualbino wakiwemo watoto waliokuwa katika kambi hizo wakati wa matukio hayo, walianza kurejea makwao baada ya hali ya usalama kuonekana kuwa imeimariska, kwa mujibu wa majarida ya Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utetezi na ustawi wa watu wenye ualbino nchini, Under The Same Sun la Septemba hadi Desemba, 2010, na la Julai hadi Septemba, 2018.

Hali ya usalama kwa watu wenye ualbino iliboreshwa zaidi kati ya mwaka 2015 hadi 2019 ambapo halikuripotiwa tukio lolote la ukatili dhidi yao hadi Novemba 2, 2022, ambapo Mkazi wa Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Joseph Mathias (50) alipouawa kwa kukatwa mapanga kisha wauaji kutokomea na mkono wake.

Tukio lingine lilitokea Mei 4, 2024, Katoro mkoani Geita, baada ya mtoto mwenye ualbino, Julius Kazungu (10) alinusurika kifo baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali na mtu ambaye hakutambulika.

Kwa mujibu wa Under The Same Sun kwa Tanzania na Afrika Mashariki, mtu mmoja katika kila watu 1,400 ana ualbino.

People are also reading