Home Back

WALIOVAMIA WAKIWA NA MAPANGA, NONDO WAUAWA KWA KUPIGWA NA KUCHOMWA MOTO SHINYANGA MJINI

malunde.com 2024/7/7

Na Mapuli Kitina Misalaba

Vijana wawili wa kiume wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameuawa baada ya kupigwa sehemu mbalimbali za miili yao kisha kuchomwa moto na watu wenye hasira kali kwa tuhuma za wizi.

Akizungumza na Misalaba Media Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP ) Janeth Magomi amethibitisha  kutokea kwa tukio hilo huku akiwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi pindi wanapowakamata wahalifu badala yake kuwawapeleke sehemu husika ikiwemo kwenye kituo cha polisi.

Kamanda Magomi amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Alhamis Juni 6,2024 katika kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga likihusisha watu wawili mmoja akifahamika kwa jina la Bahati Dotto mwenye umri wa Miaka 35 na mwenzake akijulikana kwa jina moja la Emma ambao wote wawili wameuawa kwa tuhuma za wizi.

Marehemu Bahati Dotto ni mkazi wa mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha ambaye ameuawa katika eneo la mtaa wa Iwelyangula baada ya kukimbilia ndani ya nyumba ya bibi yake ambapo Bwana Emma ni mkazi wa Bugayambelele kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.

“Leo asubuhi katika kijiji cha Iwelyangula kata ya Kitangili Manispaa na Mkoa wa Shinyanga mtu mmoja anayejulikana kwa jina Bahati Dotto mwenye umri wa Miaka 35 mkazi wa Chamaguha aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kuchomwa moto ndani ya nyumba ya bibi yake alipokuwa amekimbilia ambapo alikamatwa na kuwataja wenzake kisha akauawa na watu wenye kujichukulia sheria mkononi”.

“Tarehe hii hii leo majira ya saa tano na nusu asubuhi huko katika kijiji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi katika Manispaa na Mkoa wa Shinyanga mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Emma aliuawa ndani ya nyumba yake kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili kisha kuchomwa moto na watu wenye kujichukulia sheria mkononi baada ya kutajwa na marehemu wa kwanza, chanzo cha tukio ni baada ya marehemu wote wawili leo majira ya saa tisa za usiku kuvamia nyumba ya mtu mmoja jina lake tumelihifadhi mkazi wa kijiji cha Mwamashele wakiwa na nondo, sululu na panga kwa nia ya kutaka kumpora na kesi imefunguliwa”,amesema kamanda Magomi

SACP Magomi amesema kuwa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kufanya upelelezi ili kuchukua hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa mtaa wa iwelyangula Bwana Robert Mnyeleshi ameelezea namna alivyopokea taarifa za tukio la marehemu Bahati Dotto huku akitaja hatua alizochukua ikiwemo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.

“Taarifa hii nilipigiwa simu kwenye saa nane za usiku kwamba hapa kwetu tumezingilwa nikasema na watu gani, we njoo uwaone na kweli sikusita sikumaliza hata nusu saa nikawa nimefika kwenye tukio nimekuta watu wamejaa nikaanza kujitambulisha nikawauliza kuna nini wengine wanalielezea wengine wananiambia kama na wewe unataka kupoteza maisha endelea kukaa hapa nikaona hapa nitakufa na giza hili nikatoka nikaenda kujificha sehemu nikaanza kupiga simu kwa wahusika nikaanza kuwapigia polisi baada ya hapo nikampigia meya nikampigia na mtu mwingine mtawala wa Wilaya akasema mara moja tunakuja, nilipoona asubuhi pamepambazuka nikasogea nikakuta huyu kijana Bahati Dotto tayari ameuawa na kuchomwa moto”, amesema Mwenyekiti wa mtaa Mnyeleshi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wakiwemo majirani wameeleza namna wanavyomfahamu marehemu huyo ambapo wamesema Bahati Dotto alikuwa ni kamanda wa jeshi la jadi Sungusungu mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha ambapo pia alikuwa anajishughulisha na kazi ya kubeba mizigo kushusha kwenye gari katika soko kuu mjini Shinyanga.

Naye mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko pamoja na diwani wa kata ya Kitangili Mhe. Mariam Nyangaka wametoa pole kwenye familia zilizopatwa na changamoto hiyo akiwemo bibi wa marehemu Bahati Dotto ambapo bibi huyo ana zaidi ya Miaka mia moja na kwamba nyumba yake imechomwa moto na kuteketezwa vitu mbalimbali ikiwemo chakula.

Wakazi wa kata za Chamaguha na Kitangili wakitazama eneo ambalo ameuawa na kuchomwa moto marehemu Bahati Dotto mwenye umri wa Miaka 35 mkazi wa mtaa wa Sanjo.

Nyumba ya bibi mwenye umri zaidi ya Miaka Mia moja ambapo marehemu Bahato Dotto alikimbilia ndani na kusababisha nyumba hiyo kuchomwa moto na watu wenye hasira kali.

Diwani wa kata ya Kitangili Mhe. Mariam Nyangaka upande wa kushoto akizungumza na wananchi katika eneo la tukio.

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP ) Janeth Magomi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
People are also reading