Home Back

Wabuni mfumo wa kulipa ada kidjitali

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Dar es Salaam. Kampuni ya mtandao wa simu ya Airtel imejitosa kuunga mkono juhudi za Serikali ya matumizi ya teknolojia katika shughuli za kielimu kwa kuwawezesha wazazi kulipa ada kwa mfumo wa kidigitali.

Mfumo huo utawawezesha wazazi kulipa ada popote pale watakapokuwa kupitia simu ya kiganjani hatua inayotajwa kuwasaidia kuokoa muda, usumbufu pamoja na changamoto zilizopo katika eneo hilo.

Mfumo huo wa Airtel Money School Pay , unaongeza usalama na njia madhubuti kwa wazazi na walezi ili kuweza kufanya malipo ya ada shuleni popote nchini.

Lakini pia hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikisisitiza mifumo ya kitehama nchini kusomana sambamba na kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.

Akizungumza leo Alhamisi, Juni 27, 2024 makao makuu ya mtandao huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba amesema wazazi wana majukumu mengi ya kujenga familia zao hivyo mfumo utawasaidia kuwapunguzia usumbufu wa kupoteza muda kufanya miamala.

"Mfumo huu una huduma za ziada kama mifumo ya usimamizi wa ada, usimamizi wa wanafunzi, usimamizi na kutunza kumbukumbu za uhasibu.

"Shule binafsi kote nchini zitaweza kukusanya ada moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki, na hivyo kuwezesha njia bora katika usimamizi wao wa fedha," amebainisha.

Amesema wazazi wanaweza kuepuka foleni ndefu na kulipa ada kwa urahisi kupitia simu zao huku wakihakikishiwa miamala inafanyika kwa salama na kupunguza hatari zinazohusiana na utunzaji wa pesa.

"Airtel Money School Pay inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kufikia uchumi wa kidijitali kwa kupunguza matumizi ya fedha taslimu (cashless economy)," amebainisha.

Aidha amesema, itasaidia katika kujenga mustakabali mzuri wa sekta ya elimu nchini.

Hivyo, katika kuhakikisha hilo Airtel imeingia makubaliano na shule kadhaa za kibinafsi ikiwemo Shule za Fountain Gate, Ubungo Islamic High School, na Shule ya Sheikhat Hissa.

Mkurugenzi wa Shule ya Fountain Gate, Japhet Makau, amesema malipo ya ada kupitia mfumo huo utasaidia kuacha kutumia karatasi kwa sababu ni mfumo wa kisasa wa kufanya malipo na unaojiendesha kwa mtandao ambapo itachangia kutunza mazingira.

"Wazazi kwenda kwenye benki kulipa ada kisha kupeleka Bank Sleep ingeweza kuchukua hata siku nzima lakini hii suluhisho ataweza kulipa popote pale alipo," amesema.

"Taarifa zitakuwa kwa mpangilio mzuri na kuondoa kero ya kutunza nyaraka kwa ajili ya marejeleo kwa kuwa mfumo huu upo kidijitali.

"Wazazi na wanafunzi hawatohitaji kubeba au kuhifadhi kumbukumbu za malipo na risiti ili kufuatilia na kuhakikisha malipo yao yamefika shule," amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa shule ya Sheikhat Hissa, amesema fursa hiyo ni mwarobaini katika malipo ya karo za shule. zaidi ameomba Airtel kuusimamia vyema.

People are also reading