Home Back

Refa afariki dunia akiwa uwanjani

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Songwe. Mkoa wa Songwe umeendelea kukumbwa na matukio ya vifo vya wanamichezo uwanjani baada ya leo Julai 2, mwamuzi Hedman Mwashoga kuanguka na kufariki dunia.

Mwamuzi huyo alikuwa akichezesha mechi baina ya Monaco dhidi ya Viena FC katika uwanja wa Shule ya Msingi, Msanyila katika mwendelezo wa ligi ya kijiji cha Msanyila mkoani humo.

Hili ni tukio la tatu katika miaka miwili mfululizo, ambapo Aprili 10 2023, mchezaji Albert Andrea alipogongana na mwenzake uwanjani na kufariki dunia.

Tukio kama hilo lilitokea tena Machi 28 mwaka huu, ambapo mchezaji Bille Mgalla alianguka wakati akijaribu kufuata mpira wa juu akiwa na mpinzani wake na kuanguka na kufariki dunia.

Jana Julai 2, Refa huyo akiwa katika majukumu yake alianguka ghafla na kupoteza fahamu, ambapo alipelekwa Hospitali ya Isansa na kukutwa tayari ameshafariki.

Mmoja wa wadau wa michezo na maendeleo mkoani humo ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo, Onesmo Mkondya amesema mwamuzi huyo amefariki dunia akiwa katika majukumu yake.

"Ligi ni ya kijiji cha Msanyila na aliyetoa zawadi katika mashindano hayo ni Mkuu wa Mkoa, Daniel Chongolo na hadi sasa imefikia hatua ya robo fainali, ambapo refa huyo akiwa katika kazi yake alidondoka na alipowahishwa Hospitali alikutwa ameshafariki" amesema Mnkondya.

People are also reading