Home Back

Samia atoa ndege kusafirisha mwili wa RAS

ippmedia.com 2024/7/4
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akimfariji mke wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Dk. Tixon Nzunda.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akimfariji mke wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Dk. Tixon Nzunda.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa ndege maalum itakayoubeba mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Dk. Tixon Nzunda (56), kwenda nyumbani kwake Goba, jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya mazishi.

Aidha, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, amemwelezea marehemu Dk. Nzunda, alikuwa kiongozi wa umma mwadilifu katika kuwatumikia wananchi na kila mara alikuwa na hofu ya kuwatanguliza wananchi.

Dk. Nzunda na dereva wake, Alphonce Edson (54), walipoteza maisha Juni 18, mwaka huu, saa 8:30 mchana katika eneo la Mjohoroni (Palestina), Kata ya KIA, Wilaya ya Hai, baada ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser VXR, kugongana uso kwa uso na lori la kubeba nishati ya gesi safi, mali ya Kampuni ya Orange Gas.

Lori hilo lenye namba za usajili T 655 ABY, aina ya Scania lilikuwa likitokea Arusha kwenda Moshi.

Jana Dk. Mpango akiwa katika makazi ya viongozi wa serikali eneo la Shanty Town katika Mji wa Moshi, alikokwenda kutoa salamu za rambirambi na kumfariji mjane wa Dk. Nzunda, alisema anamkumbuka vizuri marehemu, kwa kuwa alipokuwa Waziri wa Fedha, alikuwa anakaa naye.

“Nilishtuka kidogo maana jana (juzi), niliondoka nyumbani saa tisa alasiri, na sikuwa nimepata habari yoyote. Nilipofika kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma, ndipo nilipo arifiwa kwamba mwenzetu ametangulia kupitia ajali mbaya pale karibu na KIA; na alikuwa anakuja kunipokea. Ni jambo gumu, lakini tumuombee mwenzetu.

…Nimemwomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, anifikishie salamu za pole kwa familia ya dereva wake, ambaye alifariki katika ajali ile. Natamani sana ningefika, lakini Mkuu wa Mkoa ataenda kutuwakilisha.”

"Nilikuwa nakaa naye sana marehemu (Dk. Nzunda), akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwenye vikao vyetu vya utatu na wafanyakazi; ambapo alikuwa mtu makini sana na mpole.

"Kwa upande wa serikali tukio hili limetuumiza sana. Kwa niaba ya serikali na mimi mwenyewe, Rais yupo safarini, tunasema poleni sana na niwashukuru kwa moyo wenu toka tukio hili litokee; mmekuwa pamoja na familia na huu ndio Utanzania ninaoufahamu.” 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema Juni 21 saa 4:00 asubuhi mwili wa Dk. Nzunda, utapelekwa nyumbani kwake Shanty Town na kufanyiwa ibada fupi, wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro watapata fursa ya kuuaga.

"Baadaye saa 10:00 jioni, mwili huo utasafirishwa kwa ndege maalum kuelekea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam (Goba), kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Utakapofikishwa Dar es Salaam mwili huo utalala nyumbani hapo, ukimsubiria mtoto wake aliyeko nchini India, anayetarajiwa kufika Ijumaa saa 3:00 asubuhi,” alisema maziko yatafanyika Juni 22.

Aidha, alisema mwili wa dereva wake, Alphonce Edson (54) unatarajiwa kuzikwa Julai 24, nyumbani kwake Mabogini Chekereni. 

RAIS SAMIA AMTUMIA POLE RC

Rais Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kutokana na kifo hicho.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Sharifa Nyanga, ilisema Rais Samia ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Mary Mosha

People are also reading