Home Back

Rais Samia afanya uteuzi akiigusa ofisi yake

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, huku akiigusa ofisi yake kwa kuteua watendaji wanne katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Miongoni mwa viongozi waliotoka katika ofisi ya Rais ni pamoja na Zuhura Yunus aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Felister Mdemu aliyekuwa msaidizi wa Rais, Maendeleo ya Jamii.

Wengine ni Petro Itozya aliyekuwa msaidizi wa Rais Siasa na Nehemia Mandia aliyekuwa msaidizi wa Rais upande wa sheria.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka leo Juni 6, 2024 imeeleza kuwa Rais amefanya uteuzi huo katika kuboresha utendaji kazi.

Rais Samia amemteua Stanslaus Nyongo kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji.

Uteuzi mwingine uliofanywa ni wa Naibu makatibu wakuu ambapo amemteua Zuhura Yunus kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Pia amemteua Felister Mdemu kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu anayeshughulikia masuala ya jinsia na wanawake.

Katika uteuzi huo, Amon Mpanju atakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu anayeshughukia masuala ya maendeleo ya jamii na makundi maalumu.

Katika taarifa hiyo, Balozi Kusiluka amesema Rais amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakuu wa Wilaya ambapo Petro Itozya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Nyangasa amehamishwa kutoka Wilaya ya Kisarawe kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa.

Pia, Dk Hamis Mkanachi amehamishwa kutoka Wilaya ya Kondoa kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo na kwamba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Elibariki Bajuta atapangiwa kazi nyingine.

Rais Samia pia amewahamisha makatibu tawala wa wilaya ambapo Reuben Chongolo amehamishwa kutoka Wilaya ya Songwe kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi.

Frank Sichwale amehamishwa kutoka Wilaya ya Mufindi kwenda kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Songwe.

Wakurugenzi

Uteuzi na uhamisho wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri umewagusa Mussa Kitungi ayeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Kalekwa Kasanga ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kabla ya uteuzi huo  Kasanga alikuwa Ofisa Sheria Mwandamizi, Tume ya Kurekebisha Sheria.

Shaaban Mpendu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, kabla ya uteuzi Mpendu alikuwa Mhasibu Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Sigilinda Mdemu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele. Kabla ya uteuzi huo Mdemu alikuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Rais Samia amemteua Milton Lupa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo huku akimhamisha Upendo Mangali kutoka Halmashauri ya Mji wa Babati kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.

Kisena Mabuba amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, akichukua nafasi ya Mwantum Mgonja ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Teresia Irafay amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang'.

Majaji Mahakama Kuu

Rais pia amefanya uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu kwa kumteua Nehemia Mandia kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya uteuzi huo Mandia alikuwa Msaidizi wa Rais upande wa sheria.

Projestus Kahyoza ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya uteuzi huo Kahyoza alikuwa Naibu Msajili Mwandamizi wa Masijala Kuu ya Mahakama Kuu, Dodoma.

Pia amemteua Mariam Omary kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Awali Omary alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

“Uapisho wa Naibu Waziri, Naibu Makatibu Wakuu na Majaji wa Mahakama Kuu utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye,” amesema Balozi Kusiluka katika taarifa hiyo.

People are also reading