Home Back

Polisi yaeleza ilivyomdaka aliyekuwa RC anayedaiwa kulawiti mwanafunzi

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda (46) kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Mwanza.

Taarifa za kushikiliwa Dk Nawanda imetolewa leo Alhamisi Juni 13, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alipozungumza na waandishi wa habari jijini humo.

Mutafungwa amedai kuwa mtuhumiwa amekamatwa leo saa sita mchana akiwa jijini Mwanza na yupo mahabusu kwa mahojiano.

“Jeshi la Polisi limemkamata na linaendelea kumhoji Yahya Esmail Nawanda, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Amekamatwa kwa tuhuma za kumuingilia kimwili kinyume na maumbile mwanafunzi wa kike wa chuo kikuu ambaye jina lake tunalihifadhi,” amedai Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa amedai kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024, usiku eneo la Rock City Mall wilayani Ilemela.

Amesema mahojiano ya polisi dhidi ya mtuhumiwa huyo yanaenda sambamba na kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kuzihusisha taasisi za uchunguzi wa kisayansi.

Kamanda Mutafungwa amesema uchunguzi huo utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kisha kurejeshwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ya Mkoa wa Mwanza kwa hatua za kisheria ikiwamo kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amesema mwanafunzi anayedaiwa kutendewa ukatili huo wa kijinsia anaendelea na matibabu huku akiwa chini ya uangalizi wa maofisa wa Dawati la Jinsia na Ustawi wa Jamii kwa msaada wa kisaikolojia.

“Niutake umma kuepuka kutoa taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwenye mitandao ya kijamii katika namna ambayo inaendelea kumuumiza mwathirika wa tukio la kikatili yaani mwathirika anaumia kisaikolojia kutokana na namna watu wanavyoendelea kuyaripoti matukio hayo. Utoaji wa matukio ya aina hiyo una misingi yake inayohifadhi misingi ya utu,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Taarifa ya mwanafunzi huyo kudaiwa kulawitiwa ziliripotiwa na Gazeti la Mwananchi la Juni 11, 2024.

Baada ya kuripotiwa kwa taarifa hiyo, asubuhi ya siku hiyo, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilitangaza uteuzi na utenguzi wa viongozi mbalimbali uliokuwa umefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Miongoni mwa waliotenguliwa ni Dk Nawanda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na nafasi ikachukuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi ambaye ameapishwa leo Alhamisi na Rais Samia kushika wadhifa huo.

Chanzo cha habari kilidai kuwa mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza mwenye miaka 21 alishawishiwa kufanya kitendo hicho ndani ya gari.

Chanzo kingine kutoka moja ya ofisi nyeti za Serikali jijini Dodoma, kimedai baada ya kwenda kwenye gari lililokuwa eneo la maegesho ya klabu, ndipo alipolawitiwa.

“Tunavyoambiwa sio kwamba huyo mwanafunzi aliridhia, hapana. Huyu jamaa alimtisha sana na kwa vile huyu dada alikuwa anamjua kama mheshimiwa, alijua ni watu wanatembea na silaha na walinzi hivyo akafanya aliyoyafanya.”

“Inaonekana huyu ni mchezo wake baada ya kumshawishi sana huyu dada wa watu akamgomea. Ndio naona akaja na hiyo plan B (mpango wa pili) wa kumwita kwenye gari akamvua nguo kwa nguvu na kumlawiti,” kilidai chanzo kingine.

Chanzo kingine kilidai kigogo huyo na gari alilolitumia vilinaswa na kamera za usalama zilizofungwa eneo hilo tangu gari hiyo inaingia, kuegeshwa na kutoka usiku wa saa sita na namba za usajili zilisomeka vizuri.

Kamera zinaonesha ilipofika saa 2:48 usiku, binti huyo alionekana akiingia katika gari hilo na saa 3:21 usiku, takribani dakika 30 kupita, mlalamikaji alionekana akitoka kwenye gari.

Saa 6:24 usiku, zinaonesha gari hilo lilionekana katika geti la kutokea likiwa eneo la mwanga mkali uliowezesha kulitambua usajili wake. Dereva wa gari hilo alikuwa amevalia kofia aina ya kapelo akitoka kwenye gari hilo kwa ajili ya kulipia ushuru wa maegesho.

Taarifa zinadai, Juni 3 mwaka huu, siku moja tangu alipofanyiwa ukatili huo, binti huyo alikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi dawati la jinsia na watoto, jijini Mwanza. Alisikilizwa kisha kupelekwa moja ya hospitali kubwa jijini hapo kwa uchunguzi.

Katika uchunguzi huo uliofanywa na daktari (jina tunalihifadhi), alibaini mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza aliingiliwa kinyume na maumbile.

People are also reading