Home Back

Sita mbaroni wakidaiwa kumuua mama yao mzazi

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Mwanza. Watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya mama yao mzazi, Shija Mageranya (77), mkazi wa Kijiji cha Ndua Kata ya Kasororo wilayani Misungwi mkoani humo.

Watuhumiwa hao ni Kashinja Dotto (55), Joseph Dotto (20), Magerani Dotto (44), Nyanzala Dotto (34), Masaga Dotto (46) na Milapa Dotto (30), wanadaiwa kufanya mauaji hayo baada ya kumtuhumu mama yao kuwa mshirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema leo Jumanne, Juni 4, 20 kuwa tukio hilo lilitokea Juni mosi katika kijiji hicho, watoto hao walikuwa wakimtuhumu mama yao anawaroga wajukuu zake.

"Tukio lilitokea saa 2:30 usiku, wakati bibi huyo akipata chakula cha usiku pamoja na wajukuu zake, ghafla waliingiliwa na mtu mmoja aliyewasalimia, kisha akachomoa panga na kumshambulia bibi huyo kwa kumkata sehemu za kichwani na mabegani,” ameeleza kamanda huyo.

Kamanda Mutafungwa amesema kifo cha bibi huyo kilisababishwa na kuvuja damu nyingi.

Hata hivyo, amesema baada ya mtu huyo mwanamume kutekeleza shambulio hilo, alitokomea na kuwaacha wajukuu wakimshuhudia bibi yao akikata roho.

"Chanzo cha tukio hilo ni imani potofu za kishirikina, watoto wa marehemu wamekuwa wakimtuhumu mama yao mzazi kwamba anawaroga wajukuu zake kwa kuwasababisha kupata wendawazimu na hata vifo ambavyo havieleweki katika familia yao.

“Inadaiwa walipanga njama pamoja na watu wengine ambao tunawatafuta kwa kumuua mama yao," amedai Kamanda Mutafungwa.

Wakati huohuo, Kamanda Mutafungwa amesema jeshi hilo linawashikilia vijana wawili-- Jovini Kamando (26) na Kelvin Reymond (27) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Acqulina Maltin (17), huku chanzo cha tukio hilo ikidaiwa ni wivu wa mapenzi.

“Mei 25, 2024 saa 12 alfajiri katika mtaa wa Nyamanoro Mashariki ulioko Wilaya ya Ilemela, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tulipokea taarifa kwamba binti aitwaye Acqulina Maltin (17) mkulima na mkazi wa eneo hilo alikutwa amefariki, huku mwili wake ukiwa nusu uchi na ulikuwa umetupwa uchochoroni katika maeneo ya huo mtaa. Baada ya kukagua mwili huo alikuwa na michubuko mgongoni na kwenye mkono wa kushoto," amesema.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou toure ilibainika binti huyo aliuawa na mwili wake ulikuwa na dalili za kuingiliwa kimwili.

“Baada ya kufuatilia tumewakamata watuhumiwa wawili na chanzo cha tukio hilo kulingana na taarifa tunazoendelea kupata inasemekana ni wivu wa mapenzi," amesema Kamanda Mutafungwa.

Kutokana na matukio hayo, Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuacha kuamini ushirikina, ili kuepusha kufanya mauaji kwa watu wasio na hatia.

People are also reading