Home Back

BoT kufuatilia makato malipo ya kielektroniki

mwananchi.co.tz 2024/10/5

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanza kufuatilia watoa huduma kwenye Mfumo wa Malipo ya Papo Hapo (TIPS) ambao hawajapunguza gharama wanazowatoza wateja katika huduma za malipo.

Hayo yameelezwa na Mchambuzi wa Programu za Kompyuta katika Idara ya Maendeleo ya Mifumo na Usaidizi wa BoT, Octalion Urassa alipozungumza na Mwananchi Digital katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Urassa ameyasema hayo wakati ambao hadi sasa benki zote 39 za biashara na kampuni sita za simu,zikiwemo Vodacom, Halopeasa, TTCL Azampesa, Tigo na Airtel zimejiunga na TIPS.

“Awali tulianza na mradi wa majaribio wa benki za biashara chache na kampuni ya simu, lakini sasa watoa huduma wote wameunganishwa kwenye mfumo huu, jambo ambalo litafanya miamala iwe ya uwazi zaidi na sasa tutakwenda kufuatilia ambao hawajashusha gharama,” amesema Urassa.

Hayo yanajiri baada ya BoT kutoa waraka wa ada za Mfumo wa Ulipaji wa Mabenki Tanzania (TISS) chini ya kifungu cha 56(3) cha Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa, 2015, na Kifungu cha 6 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006 iliyokuwa ikiwataarifu watoa huduma juu ya ada na tozo za TISS zilizorekebishwa.

Uhakiki huo, uliojumuisha mashauriano na wadau ni sehemu ya mipango inayolenga kupunguza gharama zinazohusiana na malipo ya kielektroniki, kukuza malipo ya kidijitali na kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Urassa, awali ili kufikia uwezo wa kufanya malipo kielektroniki, benki zilikuwa zikifanya mikataba mingi baina ya benki nyingine na kampuni za simu, hivyo kufanya mlolongo mrefu.

Amesema baada ya kuunganishwa katika mfumo wa TIPs, sasa watafanya miamala bila kuhitaji makubaliano mengi.

Hali hiyo imefanya sasa wananchi kufanya malipo ya bidhaa na huduma kutoka kwa mtoa huduma yeyote bila kuwekewa fedha katika mtandao maalumu tofauti na awali.

"Tulitoa waraka unaozungumzia upungufu wa usimamizi wa gharama kwa watoa huduma baada ya kuunganishwa kwenye TIPS. Mpango huu ulianza Januari mwaka huu na unatarajiwa kutekelezwa kikamilifu ifikapo Mei," amesema Urassa.

Akitoa maoni yake, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Dk Abel Kinyondo amesema uhifadhi fedha katika mfumo ni muhimu kwa sababu kunaruhusu ufuatiliaji.

“Hiyo inasaidia katika kuzuia ukwepaji wa kodi, na kupunguza rushwa kwa vile mfumo huwa na uwazi," amesema.

Katika hatua nyingine, BoT inatarajia kuzindua mifumo mipya ya malipo katika Mfumo wa TIPS katika mwaka huu wa fedha, unaolenga kuongeza ufanisi na usalama wa mifumo ya malipo nchini kote.

Mifumo hiyo ni pamoja na mfumo sanifu wa malipo wa msimbo wa QR, ujumuishaji wa TIPS na mfumo wa malipo serikalini (GePG) na mfumo wa ombi la kulipwa.

Katika mfumo wa malipo, Urassa amesema upo mkakati wa kuondoa namba za zamani za Lipa Namba na badala yake kuweka inayoweza kutumika kwa malipo kupitia mtoa huduma yeyote aliyeunganishwa na TIPS, kuanzia mwaka mpya wa fedha.

"Tulianzisha huu kama mradi wa majaribio mwaka jana na tunapanga kuutekeleza kikamilifu, ili kuunganisha watoa huduma wengine kwenye bidhaa," ameeleza.

Kuhusu kuunganishwa kwa TIPS na GePG, kutarahisisha uwezo wa watoa huduma kufanya malipo ya serikali bila kuhitaji akaunti za makusanyo ya mapato.

"Awali akaunti zilikuwa za lazima kwa ajili ya kupokea malipo, lakini sasa huhitaji kuwa sehemu ya mfumo wa ukusanyaji wa Serikali," amesena Urassa.

Amesema mifumo hiyo inafanya kazi ndani ya TIPS, na jitihada zinaendelea kutoa elimu kwa wadau juu ya kuweka mifumo yao kwa ajili ya matumizi ya wateja.

Kuhusu mfumo wa ombi la kulipwa deni lako, Urassa ameeleza kuwa unawaruhusu walipokea malipo ambao ni watoa huduma kama DSTV, Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuanzisha muamala wa kuomba kulipwa,  huku malipo yakikatwa moja kwa moja pale mlipaji anapokubali ombi hilo.

People are also reading