Home Back

Airtel Money yazindua huduma ya kurahisisha malipo ya ada za shule kidijitali

muungwana.co.tz 2024/10/5


Airtel Money Tanzania leo Juni 27, 2024 imezindua huduma ya malipo kidijitali ‘Airtel Money School Pay’ yenye lengo la kurahisha mchakato wa ulipaji wa Ada katika shule mbalimbali. 

Airtel Money School Pay itasaidia kuongeza usalama, na njia madhubuti kwa wazazi na walezi ili kuweza kufanya malipo ya ada shuleni ukiwa popote nchini. Huduma ya Airtel Money School Pay imeundwa mahususi kwa shule binafsi ili kurahisisha malipo na kutunza kumbukumbu wakati wowote.

Wazazi sasa wanaweza kulipa ada za shule kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi, wakati wowote na mahali popote kutokana na kuunganishwa kwa teknolojia ya malipo ya simu ya Airtel Money School Pay. Shule binafsi kote nchini zitaweza kukusanya ada moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki, na hivyo kuwezesha njia bora katika usimamizi wao wa fedha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Airtel Tanzania, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba, alisisitiza umuhimu wa huduma ya malipo ya Airtel Money School School, huku akieleza kuwa ni hatua kubwa ya kuimarisha usalama na usimamizi wa malipo shuleni, hasa kwa wazazi na shule za Tanzania.

“Tumejitolea kutoa suluhisho la kibunifu litakalorahisisha malipo baina ya wazazi, walezi na shule katika swala la ulipaji karo. Airtel Money School Pay ni mfano dhahiri wa jinsi Airtel Money inavyowapa kipaumbele wateja wake kwa kurahisisha na kuboresha maisha yao. Mfumo huu ni wa kipekee na una huduma za ziada kama Mifumo ya usimamizi wa ada, mfumo wa usimamizi wa wanafunzi, na mfumo wa usimamizi na kutunza kumbukumbu za uhasibu, Mifumo yote hiyo inatolewa bila malipo kwa shule zinazotumia mfumo huu wa Airtel Money School Pay. Wazazi wanaweza kuepuka foleni ndefu na kulipa ada kwa urahisi kupitia simu zao. Huu mfumo unahakikisha miamala inafanyika kwa salama na kupunguza hatari zinazohusiana na utunzaji wa pesa,” alieleza.

Rugamba alieleza kuwa Airtel Money School Pay inalenga kuunga mkono juhudi za serikali kufikia uchumi wa kidijitali kwa kupunguza matumizi ya fedha taslimu (cashless economy).

Rugamba aliongeza, "Airtel Money School Pay itasaidia katika kujenga mustakabali mzuri wa sekta ya elimu nchini, tunashaukuru sana kushuhudia matokeo chanya ambayo yameshaanza kutokea katika shule zetu zinazotumia mfumo huu wa Airtel Money School Pay.”  

Baadhi ya shule kibinafsi nchini zishaanza kutumia mfumo huu, ambao unawawezesha wazazi kufanya malipo ya karo ya shule. Shule hizo ni pamoja na Shule za Fountain Gate, Ubungo Islamic High School, na Shule ya Sheikhat Hissa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Fountain Gate, Japhet Makau, alitoa shukrani zake kwa Airtel Money kwa kuanzisha mfumo ambao unahakikisha usalama wa miamala ya malipo ya ada kutoka kwa wazazi na walezi.

 "Mfumo wa Airtel Money School Pay umeboresha kwa kiasi kikubwa utaratibu wetu wa kukusanya ada na pia umeimaisha usimamizi wetu wa fedha kwa kutoa muda wa kupokea uthibitisho wa papo kwa hapo ada zilizolipwa na vipengele vya ziada vimesaidia usimamizi wote bila matatizo," Makau alisema.

Aliongeza “Malipo ya ada kupitia Airtel Money School Pay inatusaidia kuacha kutumia karatasi kwa sababu ni mfumo wa kisasa wa kufanya malipo na unaojiendesha kwa mtandao; hii itachangia kutunza zaidi mazingira yetu. Taarifa zetu zitakuwa kwa mpangilio mzuri na kuondoa kero ya kutunza nyaraka kwa ajili ya marejeleo kwa kuwa mfumo huu upo kidijitali, wazazi na wanafunzi hawatohitaji kubeba au kuhifadhi kumbukumbu za malipo na risiti ili kufuatilia na kuhakikisha malipo yao yamefika shule.”

Wazazi na walezi wanaweza kupata huduma ya Airtel Money School Pay kwa kupiga *150*60#, chagua chaguo 5 (Fanya Malipo), chagua Ada ya Shule, kisha uchague chaguo la 3 (School Pay) ili kuendelea na malipo.

People are also reading