Home Back

Mzambia kunogesha mbio za magari Tanga

mwanaspoti.co.tz 2024/10/6

DEREVA muongozaji (navigator) kutoka Zambia, David Sihoka ni mmoja wa magwiji wa mbio za magari  wa daraja la juu barani Afrika wanaotegemewa kunogesha mashindano ya mbio za magari ya Advent yatakayofanyika jijini Tanga katikati ya mwezi ujao.

Sihoka, amekuwa akimuongoza dereva Muna Singh wa Zambia kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, safari hii atakuwa na dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu wakiendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 10.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mount Usambara Motorsports Club, Hussein Moor ambao ndio waandaaji wa mashindano haya, “Barabara za vumbi katika maeneo ya Pongwe, Mkanyageni na Mlamleni ziko katika hali nzuri kuwezesha madereva kufanya vitu vyao katika mashindano yanayopima ubora wa injini za magari. Nafikiri wakazi wengi wa Tanga wanasubiri kwa hamu kuona jinsi gani madereva wataonyeshana ubabe barabarani.”

Orodha ya madereva gwiji wa Tanzania ambao hadi jana walikuwa wamethibitisha kushiriki katika mashindano haya, ambayo rasmi yanajulikana kama Advent Rally of Tanzania, ni pamoja na Randeep Birdi kutoka Dar es Salaam na ndugu yake Manvir Birdi ambao wataendesha gari aina ya Mitsubishi Evo 9.

Wengine, kwa mujibu wa Moor, ni Aliasger Fazal, Akida Machai, Shaneabas Fazal na Jamal Nirmal ambaye ni maarufu mjini Tanga kama Utu.

“Orodha hii ni awali iliyotufikiia mwishoni mwa juma  hili, lakini tunategemea kupata madereva wengine zaidi mpaka kufikia mwanzoni mwa mwezi wa saba,” alitanabaisha Moor.

Moja ya vivutio vikubwa katika mashindano haya, kwa mujibu wa Moor, ni dereva Waleed Nahdi ambaye dhamira yake ni kuonyesha kipaji chake cha uendeshaji kama ilivyokuwa kwa kaka yake Samir Nahdi Shanto, ambaye ni mmoja wa ‘malegendi’ wa mbio za magari nchini waliotamba katika miaka ya awali ya 2000.

Shanto, aliyetamba na Datsun 260Z na baadaye Subaru Impreza, amedai kijana wake anaweza kufanya maajabu katika mbio za magari ya Tanga kwani amempa mafunzo ya kutosha.

Dereva muongozaji kutoka Tanga, Awadh Bafadhil naye yuko mbioni kushiriki katika mashinsdano ya Advent ambayo ni ya kufungia mwaka katika mbio za  magari msimu huu.

“Safari hii nitakuwa na Alasger Fazal, dereva chipukizi kutoka Tanga,” alisema Bafadhil ambaye  ameshiriki katika mchezo wa mbio za magari kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

People are also reading