Home Back

Vurugu polisi na wananchi: Askari ajeruhiwa, gari lavunjwa kioo

tanzaniaweb.live 3 days ago
Polisi Piccd
Vurugu polisi na wananchi: Askari ajeruhiwa, gari lavunjwa kioo

Umezuka mtafaruku kati ya polisi wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro na wananchi wenye hasira katika Kijiji cha Ubetu na kusababisha askari mmoja kujeruhiwa kichwani na gari la jeshi hilo kuvunjwa kioo.

Wananchi hao walisababisha madhara hayo wakidai askari wa jeshi hilo waliwavamia na mitutu ya bunduki wakiwa kwenye sherehe.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa amesema haukuwa uvamizi bali, askari walikuwa katika doria, baada ya kuarifiwa kungekuwepo vurugu dhidi ya mmoja wa wananchi.

Chimbuko la hasira Chimbuko la hasira hizo ni kukamatwa kwa ndugu yao, Denis Tarimo (21), muhusika wa sherehe hiyo, aliyekuwa anapongezwa kuhamia katika nyumba yake mpya.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wanasema siku ya sherehe Tarimo hakuwepo kwa kuwa alishakamatwa na jeshi hilo siku sita zilizopita.

Kwa mujibu wa mashuhuda, hasira zaidi za wanafamilia zilisababishwa na namna ndugu yao huyo alivyokamatwa, ikidaiwa alianza kufuatiliwa na gari kisha wakagonga pikipiki yake katika Kijiji cha Lessorma.

Alipoanguka, inadaiwa waliokuwemo kwenye gari hilo, walishuka na kuanza kumshambulia kwa mateke na ngumi, kisha walitokomea naye kusikojulikana.

Baada ya tukio hilo, inaelezwa ndugu zake walimtafuta maeneo mbalimbali ikiwemo katika vituo vya polisi bila mafanikio, baadaye waliarifiwa kuwa amesafirishwa kwenda Kenya, anakodaiwa alitenda uhalifu.

Kwa maneno mengine, sherehe hiyo ilifanyika bila ya uwepo wa Tarimo ambaye ndiye aliyekuwa muhusika mkuu, kwa kuwa alishakuwa mikononi mwa polisi wa Kenya.

Mashuhuda Baadhi ya wananchi wameieleza Mwananchi, kuwa baada ya vurugu hizo kutokea, polisi walilazimika kupiga risasi za moto hewani kuwatawanya wananchi waliokuwepo kwenye eneo hilo.

Hata hivyo, baada ya watu kutawanyika, polisi walirudi kwenye eneo la sherehe na kumwaga pombe aina ya mbege na kuondoka na baadhi ya vitu.

Watu kadhaa wanadaiwa kushikiliwa na polisi kufuatia vurugu hizo. Tekla Andrea, mmoja wa waliokuwepo katika sherehe hiyo, anasema polisi waliingia kwa fujo wakiwa na bunduki.

"Siku ya Ijumaa alikamatwa kijana mmoja na watu wasiojulikana na wakati anakamatwa, Jumapili alipanga kufanya sherehe ya kuzindua nyumba yake mpya. Baada ya kukamatwa ndugu zake walimtafuta vituo vyote vya polisi  hawakumpata, baadaye tukaambiwa amepelekwa Kenya," amesema.

Amesema licha ya kukamatwa, familia ilikubaliana sherehe hiyo iendelee kwa kuwa tayari maandalizi yalishafanyika.

"Jumapili tuliendelea na sherehe kama kawaida, ilipofika jioni likatokea gari la polisi hadi kwenye eneo la sherehe, gafla risasi zikapigwa juu, kukawa kumetokea vurugu na baadhi ya watu waliokuwepo kwenye sherehe walikimbia," anasimulia.

Shuhuda mwingine, Anania Josephat amesema hasira ya wananchi ilitokana na namna Tarimo alivyokamatwa kufuatwa kwa utaratibu, hali iliyoonekana kama uonevu kwenye jamii.

"Wananchi wanahoji, huyu mtoto kama alikamatwa kiutaratibu kwa nini asikabidhiwe kwa polisi wa Tanzania au akapelekwa Kituo cha Polisi Tarakea, ni kwa nini alikamatwa kimyakimya na kupelekwa Kenya?" amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ubetu, Siprian Tarimo amesema amearifiwa polisi waliingia kwa fujo na silaha kwenye sherehe hizo na ndiyo chanzo cha vurugu.

"Kuna polisi walikuja nyumbani kwa mtu ambaye alikuwa na sherehe na kuingia ndani na gari lao na hawakueleza chochote, kukawa kumetokea sintofahamu, vijana waliokuwepo kwenye ile sherehe waliwashambulia kwa madai ya kuwaingilia kwenye sherehe kwa fujo," amesema.

Hata hivyo, amesema hakuwa na taarifa za awali kuhusu doria ya askari hao wala tuhuma na mpango wa kumkamata Tarimo.

"Sikushirikishwa, wala sikupata taarifa yoyote ya polisi kuhusu ukamataji wa huyu kijana. Kwa hiyo nasikia huyu kijana alitoka zake sokoni kununua mahitaji kwa ajili ya sherehe yake na wakati anatoka sokoni ndipo alipovamiwa na kukamatwa,” amesema.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala amesema tukio hilo "lipo kwenye uchunguzi, siwezi kulizungumzia kwa sasa, lakini taarifa za awali ni kwamba askari wetu mmoja alijeruhiwa na gari la polisi lilivunjwa kioo."

Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kilimanjaro, amesema askari hao walienda kuzima vurugu zulizopangwa dhidi ya mwananchi mmoja, anayedaiwa kutoa taarifa polisi hadi kukamatwa kwa Tarimo.

"Taarifa tulizozipata ni kwamba kuna kijana Mtanzania ambaye wanadai amemchongea Tarimo kule Kenya na amekamatwa, vijana wakakusanyika kutaka kufanya fujo kwenye ule mji wa mtoa taarifa. Baada ya polisi kupata hizi taarifa tulikwenda kuimarisha ulinzi na kuzima vurugu, lakini tunaendelea kuchunguza ni nini kilichotokea,” amesema.

Alipoulizwa ni utaratibu gani ambao unaruhusu mtuhumiwa aliyefanya tukio nchi jirani kukamatwa hapa nchini, RPC Maigwa alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa kuwa linahusisha Polisi wa Kimataifa (Interpol) na tukio lilifanyika nchini Kenya

"Hilo mimi siwezi kulizungumzia kwa kuwa linahusisha nchi mbili, hivyo lipo kwenye uchunguzi," amesema Kamanda Maigwa

People are also reading