Home Back

Bosi TRA ato Bosi TRA atoa msimamo

habarileo.co.tz 2024/10/6
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Mwenda

ZANZIBAR – KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Mwenda amesema yeye ni mtu wa vitendo na anamwamini Mungu atamsaidia kutimiza matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan. Ametoa kauli hiyo ya kwanza tangu kuteuliwa kwake na Rais kushika wadhifa huo.

Alikuwa akizungumza mjini Zanzibar jana wakati akiagwa na menejimenti na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Alisema yeye ni binadamu alikuwa na dhamira ya kuifanya ZRA iwe taasisi bora ya kikodi Afrika. “Mama (Rais Samia) jana ameniambia nibadilishe sura, niko hivi lakini niko ‘firm’ (makini sana), naamini sina vita na mtu lakini nina kazi ya kusimamia misingi na ukweli na nikiisimamia, naisimamia,” alieleza Mwenda.

Alisema kuna watu akiwa ZRA aliwakwaza katika utendaji hususani alipokuwa akifanya mabadiliko kuna watu walikuwa na nafasi wakakosa, waliokuwa juu walishushwa, kuna waliokuwa na huzuni na wengine furaha. “Ila nawaomba kama kuna watu nimewakwaza naomba radhi sikukusudia.

Isije ikafikia mahali nikija kufanya mazungumzo, ukasema huyu kamishna alikuwa mbaya sana alinishusha cheo, hapana mimi naamini katika kutenda kazi hata uwe rafiki yangu kama haufanyi kazi, haufanyi kazi tu,” alieleza.

Alisema kwa waliomkwaza ni jambo la kawada katika kazi na amewasamehe kwa kuwa wote ni sehemu ya ndugu na familia yake akiwa Zanzibar. Alisema namna pekee kwa ZRA kumfanya awe na furaha ni kuendeleza aliyoyafanya. Aliishukuru Serikali ya Zanzibar akiwemo Rais Dk Hussein Mwinyi, menejimenti ya ZRA na wafanyakazi kwa kumuongoza kufikia alipo.

“Pia, nawashukuru sana wafanyakazi wa ZRA kwa kweli nawapenda sana.

Nyie ndio nilikuwa nawa push muende mitaani, nyie ndio nilikuwa nawatishia ukichukua rushwa huna kazi, nyie ndio nilikuwa nataka baadaye muwe viongozi wa hii taasisi na yote hayo mmeyafanya mkiwa na hali ngumu,” alisema.

Alimshukuru Rais Dk Mwinyi kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo ingawa alisema kwa utani kuwa anasikitika maslahi yameboreshwa lakini hatakuwepo.

“Najua speed yangu wakati mwingine ilikuwa kubwa wengine mlizoea muende mkakae na familia, kuna wakati nilisikia wanasema huyu jamaa kwa sababu mkewe hakai hapa ndio maana anatuweka hapa hadi usiku.

Kweli mke wangu hakai hapa lakini kwa kufanyakazi ZRA ilikuwa inatishia uhai wa ndoa yangu,” alisema.

Alisema muda wake ulikuwa unaisha Machi lakini haukuongezwa lakini kwa kuwa sheria ilikuwa inaruhusu kuongezwa alifikiri angeongezewa muda hivyo pamoja na kwamba anaondoka lakini hatawaacha watumishi wa ZRA.

People are also reading